Maonesho ya Ujasiriamali IAA Mwaka 2023

Mkurugenzi wa masomo ya Astashahada, stashahada na shahada wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Bi Gloria Kimburu ameipongeza idara ya usimamizi wa biashara (IAA) kwa kuibua vipaji vya ujasiriamali kutokana na elimu wanayoitoa darasani kwa wanafunzi na kuonesha kwa vitendo.

Bi Gloria ameyasema hayo leo Februari 16, 2023 katika maonesho ya ujasiriamali (Entrepreneurship Exhibitions) yaliyofanyika katika Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA), pia amewashauri wanafunzi walioshiriki katika maonesho hayo kuwa na desturi ya kujisomea vitabu mbalimbali ili kuongeza maarifa juu ya ujasiriamali.

Mkuu wa idara ya usimamizi wa biashara Dkt. Martin Dome amesema kuwa kama idara wanajivunia kuanzisha kozi ya usimamizi wa utaali na uanagenzi ambayo ndio chanzo cha maonesho hayo.

Dkt. Martin ameongeza kuwa ‘’tumeona umuhimu wa kuongeza baadhi ya lugha za kimataifa tofauti na kiingereza kinachotumika sasa, katika Mtaala wa Usimamizi wa utalii na uanagenzi hivyo tutakapokuwa tunafanya mapitio ya mtaala tutaona namna ya kuongeza lugha hizo ili wanafunzi wetu waweze kuwafakia watu wengi duniani’’

Naye Bw. Bakiri Angalia akiwasilisha mada amewaasa wanafunzi kuwa wabunifu kwa kuboresha mawazo mbalimbali ya biashara na kutumia teknolojia iliyopo katika mazingira yao ili kupunguza gharama za uendeshaji katika biashara zao.

Bw. Elia Mbise mratibu wa maonesho hayo amesema; ’’Nimewafundisha namna ya kupata wazo la biashara, kutambua fursa za biashara, namna ya kuandaa mipango ya biashara na jinsi ya kutangaza biashara zao, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uwezo wa kufanya biashara na kushindana katika soko’’.

Mwita mwagori mshiriki wa maonyesho ameuomba uongozi wa chuo kuwaunga mkono kwenye biashara zao kwa kununua bidhaa wanazotengeneza pamoja na kuwawezesha katika mawazo ya biashara waliyonayo; ili waweze kufika mbali kibiashara kwa kuwa baadhi yao wamefanikiwa kufungua makampuni mbalimbali.

Maonesho haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu mwaka 2019 ambapo mwaka huu yameshirikisha wanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya usimamizi wa utalii na uanagenzi (Bachelor degree in tourism and hospitality management with apprenticeship).