Warsha Ya Mapitio Ya Mitaala Nchini

Serikali imedhamiria kufanya mapitio na kuhuisha mitaala katika Vyuo vya elimu ya juu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ili wataalam watakapohitimu masomo wawe na uwezo wa kujiajiri na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, katika ufunguzi wa Warsha ya siku  nne ya  Mapitio ya Mitaala ya Vyuo vya Elimu ya Juu, inayofanyika katika Chuo cha Uhasibu Arusha. 

Amesema warsha hii imewakusanya wataalam kutoka Vyuo mbalimbali vya elimu ya Juu hapa nchini kujadili  namna bora ya kufanya mabadiliko ya mitaala ambayo ipo katika vyuo vyao, ili mitaala hii itakapoandaliwa vijana waweze kuajiriwa na kujiajiri wenyewe na kutumia rasilimali zilizopo katika mageuzi ya kiuchumi.

“ Vijana wengi wa vyuo vyuo vya elimu ya juu wanajifunza lakini wanashindwa kuajirika, hivyo ipo haja ya kupitia upya mitaala, hata Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kupitia Wizara ya Elimu kwamba kuwe na mapitio, ambayo itawafanya vijana waweze kuajirika na kujiajiri pia,” alisisitiza Dkt. Mwaitete.   

Mratibu Msaidizi wa Mradi wa HEET, Dkt. Evaristo Mtitu amesema kupitia mradi huu taasisi za elimu ya juu zinaenda kuhuisha mitaala iliypopo na kuunda mitaala mipya ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wanaosoma mitaala hiyo kupata elimu ujuzi na stadi za maisha za kukabiliana na mazingira popote ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa mradi huu utatekelezwa kwa miaka mitano huku malengo yakiwa ni kujenga na kukarabati miundombinu, kusomesha wanataaluma (Shahada ya Uzamili na Uzamivu), kuimarisha matumizi ya TEHAMA na kupitia mitaala iliyopo na kuunda mitaala mipya kwenye maeneo ya kipaumbele ya nchi ili ijielekeze katika kutoa elimu ujuzi.

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa thamani ya dola za Kimarekani  milioni 425 kwenye vyuo vyote vikuu vya Serikali , vyuo vitano ambayo viko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango  pamoja na taasisi ambazo zinasaidia uendeshaji wa elimu ya juu nchini, zikiwemo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)  na Tume ya Sayansi.