Mahafali Ya 24 Chuo Cha Uhasibu Arusha IAA

Mkaguzi mkuu wa Ndani wa serikali Bw. Athuman Mbuttuka  ameupongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuanzisha mafunzo ya uanagenzi (apprenticeship) katika fani za utalii, fedha na bima, yatakayowawezesha  wahitimu kupata ujuzi na utaalam kutoka kwenye soko na kumudu mahitaji ya soko, kijamii na kiuchumi.

Mbuttuka ameyasema hayo leo tarehe 16 Desemba katika mahafali ya 24 ya Chuo Cha Uhasibu Arusha yaliyofanyika katika ukumbi wa AICC Arusha, ambapo amewatunuku astashada, stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili katika fani mbalimbali akimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba. 

“Ni matumaini yangu kuwa vyuo vingine nchini vitaiga mfano huu mzuri katika kuboresha mitaala yao, ili Taifa liwe na wahitimu wenye stadi shindani watakaokabiliana vema na mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya sasa,” alisema Mbuttuka.

 Aidha, Mbuttuka ametoa rai kwa vyuo vyote nchini kuhuisha mitaala yao katika fani za biashara na uongozi kuhakikisha fani hizo zinajumuisha stadi za TEHAMA na kuweka mkazo kwenye mafunzo ya akili isiyo asili (artificial intelligence), ili wahitimu wa fani za biashara, uhasibu na ukaguzi wawe na stadi zinazohitajika katika soko la dunia ya leo.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo-IAA, Dkt.Mwamini Tulli amesema kumekuwa na ongezeko la wahitimu kutoka 2,481 mwaka 2020/2021 mpaka 3529 mwaka 2021/2022, huku akiwaasaa wahitimu kuondokana na dhana ya kuajiriwa pekee badala yake wajiamini kutumia elimu waliyopata katika kupambana  na maisha.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo IAA, Dkt. Cairo Mwaitete amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukiwezesha Chuo kupata fedha za Mradi wa HEET kiasi cha shilingi bilioni 44 kwa ajili kuboresha miundombinu, kuboresha na kuhuisha mitaala na kuwaendeleza watumishi kuelimu.

Dkt. Mwaitete ameongeza kuwa kutokana na uboreshwaji wa miundombinu unaoendelea kupitia fedha za ndani,  kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi kutoka 3000 katika mwaka wa masomo 2017/18 kufikia wanafunzi zaidi ya 13,000 mwaka 2022/23.

Stanslaus Ismail mwakilishi wa Wahitimu wa masomo ya Shahada ya Uzamili, ameushukuru uongozi wa IAA kuhakikisha wanakuwa mahiri katika utafiti, kuimarisha miundombinu ya TEHAMA iliyowawezesha kusoma, kufanya mitihani huku akibainisha namna walivyoandaliwa kujiajiri kupitia Kiotamizi (Business Start Up Center).

Jumla ya wahitimu 3529 wametunukiwa astashada, stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili katika mahafali ya 24 ya Chuo Cha Uhasibu Arusha iliyofanyika katika ukumbi wa AICC Arusha.